Tuesday, August 2, 2011
'KUTAHIRI NI NJIA MOJAWAPO YA KUEPUKANA NA UKIMWI'
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inasema kuwa wanaume ambao wametahiriwa huepuka, kwa kiasi kikubwa, kupata maabukizo ya HIV/AIDS
TANGU kugundulika kwa ugonjwa wa UKIMWI mwaka 1983 hapa nchini, wataalamu mbalimbali wa masuala ya afya kote duniani wamekuwa wakihaha kutafuta tiba yake yake bila mafanikio yeyote.
Juhudi za wataalamu hao hazijaweza kuleta tiba ya ugonjwa huo ambalo ni janga la kitaifa hapa Tanzania kwani tayari watu wengi wamekufa au kuathirika kwa namna moja au nyengine na ugonjwa huo.
Katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, mbinu mbalimbali zimekuwa zikihimizwa, mojawapo ni kujiepusha na zinaa moja kwa moja, ingawa matumizi ya kondomu yamekuwa yakisisitizwa zaidi na wataalamu hao kama njia mbadala.
Lakini siku za hivi karibuni, wana sayansi wamekuja na mbinu nyingine ya kupambana na UKIMWI.
Nayo ni kwa wanaume kutahiri ili kujikinga na maambukizi ya UKIMWI.
Wanasema njia ya kutahiri wanaume imethibitishwa kuwa inapunguza maambukizi ya UKIMWI kwa asilimia khamsini na inamuepusha mwanamume na madhara mengine ya ngono.
Kutahiri ni njia ya kitaalamu inayofanywa kwa wanaume kuondoa sehemu ya ya ngozi ya uume (govi) ambayo kuweko kwake husababisha uchafu kugandiana na hivyo kuzaa wadudu.
Kongamano la wataalamu wa UKIMWI lililofanyika hapa Dar es Salaam hivi karibuni na kuwahusisha madaktari, wauguzi na wahudumu wa wagonjwa wa UKIMWI majumbani kutoka wilaya zote za mkoa wa Pwani lililenga, pamoja na mambo mengine, kuonesha hatua iliyofikiwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI mkoani humo.
Akifungua kongamano hilo Bwana Henry Clemens, Mkuu wa Wilaya ya Mkurunga anasema utafiti uliofanywa hivi karibuni katika nchi za Kenya, Uganda na Afrika ya Kusini barani Afrika, umethibitisha kuwa kutahiri kunapunguza kasi ya kuenea kwa UKIMWI miongoni mwa wanaume wakati wa kujamiiana.
“Utafiti huo umeonesha kuwa kutahiri kuna mkinga mtu na maambukizi ya UKIMWI kwa kiasi kikubwa na hivyo wataalamu hao wakapendekeza kampeni ifanyike kwa wale wote ambao hawajatahiriwa wafanye hivyo mara moja,” anasema.
Anafafanua kuwa utafiti huo pia uligunduwa kuwa maeneo ambayo watu wengi wana kawaida ya kutahiri, ina kasi ndogo sana ya maambukizi ya UKIMWI ikilinganishwa na maeneo ambayo hawatahiri kabisa.
Anawaaasa wakazi wa mkoa wa Pwani kuendeleza mila ya kutahiri ili kupunguza kasi ya maambukizi na wakati huo huo anatahadharisha njia zingine zitumike kama vile matumizi ya kondomu na kujiepusha na zinaa kuwa ni njia sahihi za kupambana na UKIMWI.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
TUWE TAYARI KUTAHIRIWA ILI MAAMBUKIZO YA HIV/AIDS YAPUNGUE NCHINI
ReplyDelete