Sheikh Twalib Ahmed, mwanzo kulia, akiwa na masheikh wenzake jijini Dar es Salaam hivi karibuni
IMAMU Mkuu wa Msikiti wa Al-Maamur uliopo Upanga jijini Dar es Salaam Sheikh Twalibu Ahmed amekemea vikali tabia ya baadhi ya waumini wa Kiislamu kujihusisha na vitendo vya ushirikina, uchawi na ndumba wawapo misikitini kwani vitendo hivyo vinamchukiza sana Mwenyezi Mungu.
Amesema ushirikina misikitini ni laana na yeyote anayejihusisha na tabia hiyo ajue kuwa anatenda madhambi na madhara yake ni makubwa mno hapa duniani na kesho akhera.
Sheikh Twalibu alikuwa akitoa nasaha zake kwa waumini wa dini hiyo jana jijini Dar es Salaam mara tu baada ya swala ya adhuhuri kufuatia kitendo cha muumini mmoja ambaye hakujulikana kuitupa hirizi yake msikitini humo kwa nia ya kuwaroga viongozi wa Msikiti huo ili wafe.
Hirizi hiyo iliokotwa na mfanya usafi wa msikiti huo na kuikabidhi kwa Sheikh Twalibu kwa hatua muafaka kwani aliogopa hata kuiguza kwa kuhofia asije akadhurika.
“Jamaani waislamu tunakwenda wapi ?” alihoji Sheikh Twalibu na kuongeza: “Msikiti ni nyumba safi, tukufu na ni mahali patakatifu pa kuabudia na kumcha Mwenyezi Mungu peke yake na vitendo vya ushirikina namna hii havina nafasi katika Uislamu.”
Alionya kuwa mwenye kujihusisha na uchawi kwa nia ya kumroga Imamu au mtu mwingine hapo Msikitini ni haramu na mtu huyo anajisumbua tu, kwani harogeki namna hiyo.
Aliongeza kusema kuwa vitendo mfano huo ni vingi msikitini hapo na kwa kweli vinaudhi na kuchukiza hata kuvisema.
Alisema kwa muda mrefu amekuwa akiletewa mashtaka juu ya vitendo vya ushirikina na mara zote amekuwa akivipuuza kwa kuwa ni vya aibu kwa mtu anayejiita mwislamu safi.
Alisema tukio la jana ni la aibu mno na ameamua kulisemea ili muimini aliyefanya kitendo hicho kwa kutumwa na mtu aviache kwani madhara ya kitendo hicho yatamrudia mwenyewe au yule aliyemtuma.
“Sielewi lengo la mtu kutupa hirizi msikitini, anataka mimi Imamu nife au anataka niondolewe msikitini achukue yeye uimamu au nini hasa?” Alihoji Sheikh Twalibu kwa ghadhabu.
Aliendelea kusema kuwa uimamu si lele mama, unataka elimu ya dini, tena kwa kusoma na si vinginevyo.
Alisema iwapo mtu ana dukuduku lake, aende kwake au kwa kamati ya msikiti akatoe dukuduku lake na si kwa njia ya mkato ya kutaka kumroga mtu kwa chuki zake tu.
Sheikh Twalibu aliwataka waislamu kudumisha upendo na umoja miongoni mwao ili uislamu uheshimiwe na wala si kwa kurogana kwa ndumba na mahirizi ambayo hayana maana yeyote katika jamii yetu.

I love you Dad!
ReplyDelete