Katika salamu za rambirambi, Kampuni ya New Habari 2006 Ltd imeahidi kumlipa mke wa marehemu Mwakiteleko mshahara ya kila mwezi kwa miaka mitano, kusomesha watoto wake wawili na watoto wa marehemu kaka yake hadi Chuo Kikuu.
Rostam Aziz, mmiliki wa New Habari Corporation, wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, The African, Dimba nk. ameahidi kuiangalia familia ya al-marhum Danny Mwakiteleko kwa karibu zaidi, ikiwemo kuwasomesha watoto wawili wa kaka yake aliokuwa akiishi nao hadi elimu ya chuo kikuu.
Rostam alisema kuwa marehemu Mwakiteleko alikuwa msikivu, mwajibikaji na mchapa kazi na kabla ya kifo chake alikuwa akiandaa toleo maalumu la miaka 50 ya Uhuru, hivyo anastahiki kukumbukwa kwa yale yote aliyoyafanya.
Marehemu Mwakiteleko alipata ajali Jumatato iliyopita saa 4:00 usiku katika eneo la TIOT, Tabata baada ya kukonga lori kwa nyuma wakati akitokea kazini kwenda nyumbani kwake Tabata Chang'ombe, na kufanyiwa upasuaji wa kichwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambao mauti yalimkuta Jumamosi alfariki.
Mwili wa marehemu Mwakiteleko ulisafirishwa jana kwenda Mwakaleli Tukuyu, Mbeya ambako anatarajiwa kuzikwa leo.
Marehemu ameacha mke na watoto wawili.
Mtendaji Mkuu wa New habari 2006 Ltd, Bw. Hussein Bashe alisema mtoto wa kwanza wa marehemu Mwakiteleko anayesoma kitado cha tatu na mdogo wake anayesoma darasa la sita watapewa heshima kama baba yao alivyofanya kazi kwa uadilifu katika kampuni hiyo.
Jukwaa la wahariri katika salamu zao zilizosomwa na Bw. Manyerere Jackton zilisema marehemu ameacha funzo kubwa kwa wanahabari kujituma kwani kwa namna ya pekee anastahili kupata waombolezaji wengi kama walivyokuwa jana kutokana na tabia yake ya kupenda kazi.
Katika salamu mbalimbali zilizotolewa Waziri wa Habari, Michezo na Vijana Bwana Emmanuel Nchimbi, ambaye aliyemwakilisha Rais Kikwete katika hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Danny Mwakiteleko alisema amesikitishwa sana na kifo hicho na akaahidi kuwa Ikulu nayo kwa upande wake, itatoa mkono wa pole kwa familia hiyo.
Wengine waliotoa rambirambi zao ni Jukwaa la Wahiriri sh. 3,320,000, CRDB sh. mil. 1, NHC sh. 700,000, PPF sh. 500,000, Jeshi la Polisi Tanzania sh. 200,000 Kamati ya Nishati na Madini sh. 500,000; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe alitoa sh. 200,000 na Sport FM ya Dodoma sh. 100,000 na TANESCO sh. 500,000.
No comments:
Post a Comment